Maafisa wa polisi waimarisha vita dhidi ya mihadarati

Tom Mathinji
2 Min Read
Polisi waimarisha vita dhidi ya mihadarati.

Maafisa wa polisi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, mwishoni mwa wiki, walinasa mihadarati na dawa za kulevya  baada ya msako mkali uliotekelezwa katika sehemu mbali mbali za nchi.

Katika barabara kuu ya Migori-Sirare, maafisa hao walimfumania mwendeshaji wa pikipiki aliyekuwa na magunia mawili ya bangi yenye uzani wa kilo 73.6, na ya thamani ya shilingi milioni 2,208,000. Hata hivyo mwendeshaji huyo wa pikipiki alitoroka na kuacha nyuma bangi hiyo na pikipiki yake.

Katika barabara ya Nambale-Busia, maafisa wa asasi mbali mbali walisimamisha gari aina ya pick-up lenye nambari za usajili KBM 098P, ambapo mshukiwa mwenye umri wa miaka 20 alinaswa na misokoto 350 ya bangi, yenye thamani ya shilingi 660,000.

Maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria katika barabara ya  Mai Mahiu-Nairob, walisimamsha gari lenye nambari za usajili KDN 081H, lakini dereva alikaidi amri ya kusimama, hatua iliyosababisha maafisa hao kumwandama.

Dereva huyo John Otero Mochoge, alitiwa nguvuni akiwa na mizigo 19 iliyokuwa na bangi.

Wakati huo huo, maafisa wa polisi katika kaunti ya Busia, walimshika Bertha Anyango Wandera mwenye umri wa miaka 29, katika kituo cha magari cha Busia, alipokuwa akiabiri gari kuelekea Nakuru.

Mshukiwa huyo alinaswa na mzigo wa kilo 17.15 uliokuwa na bangi yenye thamani ya shilingi 514,500.

Idara ya DCI imeelezea kujitolea kwake kuimarisha vita dhidi ya mihadarati, huku ikitoa wito kwa umma kusitisha biashara hiyo haramu.

TAGGED:
Share This Article