Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, imekamilisha zoezi la siku tatu la kutoa mafunzo kwa maafisa wa usajili wa wapiga kura, huku ikijiandaa kuzindua zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura siku ya Jumatatu.
Akizungumza wakati wa warsha ya kufunga zoezi hilo, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon aliwataka maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kudumisha uaminifu.
“Nyinyi sasa ni sehemu ya IEBC, na pia mabalozi wake, tekelezeni majukumu yenu kwa njia ya uaminifu,” alisema Ethekon.
Mwenyekiti huyo alielezea kujitolea kwa tume hiyo kuhakikisha mchakato wa uchaguzi ambao ni jumuishi ana ulio na uwazi, huku ikilenga kupeleka huduma zake karibu na wananchi.
Mnamo siku ya Jumatatu Machi 30,2026, IEBC itazindua usajili endelevu wa wapiga kura utakaodumu kwa siku 30 katika vituo vyote 59 vya Huduma.
Kulingana na tume hiyo hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wengi wanasajiliwa kuwa wapiga kura kutokana na upatikanaji kwa urahisi wa huduma hizo.