Maafisa wa idara ya makosa ya jinai DCI, wamewatia nguvuni washukiwa watatu wanaohusika na biashara haramu ya dhahabu ghushi.
Watatu hao waliokamatwa katika eneo la Westlands Jijini Nairobi, wanadaiwa kuwatapeli wakenya wawili dola 400 za kimarekani.
Martha Mwikali Katumo, James Mwenda na Calvin Onyango Magak, pia walipatikana na kilo 10.2 za dhahabu bandia na mashini moja ya kupima uzani.
Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa wafanyabiashara hao walitambulishwa kwa matapeli hao kupitia raia mmoja wa Namibia.
Kulingana na maafisa hao wa DCI, biashara hiyo pia ilimhusisha mtaalu mmoja wa uchimbaji madini, mwanajiolojia na anadaiwa alifanyia uchunguzi shehena ya kwanza ya kilo 5 za dhahabu,na kutaja kuwa ni halali.
Huku uchunguzi ukiendelea, idara ya DCI imewahimiza wakenya kuwa makini wanapojihusisha katika biashara ya dhahabu, ili kuepuka kutapeliwa.