Maafisa wa DCI wakamata vileo ghushi Kiambu

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI wametangaza kukamatwa kwa vileo ghushi katika nyumba moja ya makazi katika eneo la Kirigiti kaunti ya Kiambu.

Kitengo cha kuchunguza makosa ya kiuchumi na kibiashara kutoka DCI kwa ushirikiano na maafisa wa shirika la kukusanya ushuru nchini KRA walitekeleza msako huo jana Jumamosi.

Walipata zaidi ya chupa 3,800 za pombe ghushi zenye nembo za Chrome, Kibao, Aquila na Trace pamoja na vijikaratasi elfu 24 bandia vya idhinisho la KRA.

Lita 260 za kemikali aina ya Ethanol ambayo hutumika kutengeneza pombe zilipatikana pamoja na gunia kadhaa za vifuniko na chupa tupu 3440.

Thamani ya pombe hiyo ghushi inakisiwa kuwa shilingi milioni 7,836,500 na biashara hiyo haramu ingeikosesha serikali ushuru ziada wa thamani wa shilingi milioni 1,253,840 na ushuru wa bidhaa zilizoundwa nchini wa shilingi milioni 2,774,551.49.

Vitu hivyo vilipelekwa kwenye bohari la shirika la kukusanya ushuru nchini KRA huku maafisa wa usalama wakianzisha msako wa kumkamata mshukiwa ambaye alitoweka.

TAGGED:
Share This Article