Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kuandaliwa Meru

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kesho Ijumaa, Disemba 1, 2023, ataongoza sherehe ya kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani katika uwanja wa michezo wa Kinoru, kaunti ya Meru.

Atasaidiana na Gavana wa jimbo la Meru Kawira Mwangaza kuongoza maadhimisho hayo ambayo kaulimbiu yake mwaka huu ni, “Achia jamii ziongoze”.

Kaulimbiu hiyo inaangazia umuhimu wa mashirika ya kijamii na jukumu muhimu ambalo yanatekeleza katika kuendeleza na kuimarisha vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Wakenya wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria maadhimisho hayo.

Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa Disemba mosi, na ilitengwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuhamasisha watu kuhusu janga la ukimwi.

Agosti 1987, James W. Bunn na Thomas Netter, maafisa wa habari wakati huo katika shirika la kimataifa kuhusu ukimwi ambalo sasa linaitwa UNAIDS, walijiwa na wazo la kuwa na siku kama hiyo na walipomjuza mkubwa wao, akalikubali na kuliidhinisha.

Siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka tangu mwaka 1988.

Share This Article