M23 yajitoa kwenye mazungumzo ya amani ya Angola

Tom Mathinji and BBC
2 Min Read
Kiongozi wa jeshi la M23 Sultan Makenga.

Kundi la waasi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limetangaza kuwa halitashiriki tena katika mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika leo Jumanne Jijini Luanda, Angola.

Awali kundi hilo lilithibitisha kuwa litahudhuria kwenye mazungumzo hayo ya kwanza ya ana kwa ana pamoja na serikali ya Kongo, ambayo yenyewe inasema itahudhuria mkutano huo wa Luanda unaosimamiwa na Angola.

Kujiondoa kwa M23 katika mazungumzo hayo kumekuja baada ya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kwa kiongozi wake na makamanda wa jeshi la Rwanda.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, Msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka aliandika, “Vikwazo vilivyofuatana vilivyowekwa kwa wanachama wetu, vinaathiri kwa dhati mazungumzo ya moja kwa moja na kuzuia maendeleo yoyote,” Kanyuka alisema, akiongeza kuwa kwa sababu hizo, M23 haiwezi “kushiriki tena katika majadiliano”.

Mapema siku ya Jumatatu, Kanyuka aliripoti kuwa wajumbe wa M23 walikuwa wameshakwenda katika mji mkuu wa Angola, Luanda.Wakati M23 wakisusia, ujumbe unaoiwakilisha DRC uko Luanda tayari kwa mazungumzo, msemaji wa Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliambia shirika la habari la AP na kunukuliwa na Aljazeera, kwamba wenyewe watashiriki mazungumzo.

M23 ni mojawapo ya makundi yapatayo 100 yenye silaha ambayo yamekuwa yakigombea eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC, karibu na mpaka na Rwanda. Mzozo huo umezua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao, huku watu 7,000 wakiripotiwa kufariki tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

M23 inaungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda, kulingana na Umoja wa Mataifa. Lakini Rwanda inasema kuwa vikosi vyake vinafanya kazi ya kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoishambulia Kigali. Ikulu ya Angola ilitangaza kwa mara ya kwanza mipango ya mazungumzo hayo Machi 11 baada ya mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *