Lookman na Banda watawazwa bora tuzo za CAF

Dismas Otuke
2 Min Read

Mshambulizi wa Nigeria, Ademola Lookman, na mshambulizi wa Zambia, Barbra Banda, ndio wanandinga bora wa mwaka 2024, kwenye tuzo za Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, zilizoandaliwa Jumatatu usiku katika mji wa kitalii wa Marrakech nchini Morocco.

Hafla hiyo ya kukata na shoka ilihudhuriwa na nyota wengi wa kabumbu waliostaafu na wale wangali uwanjani.

Lookman alitawazwa mchezaji bora wa mwaka baada ya kuwa na msimu wa kufana na klabu yake ya Atalanta nchini Italia na pia timu ya taifa ya Super Eagles ya Nigeria, ikiwa mara ya pili kwa Nigeria kunyakua tuzo hiyo kwa mpigo baada ya Victor Osimhen kuinyakua mwaka jana.

Nwanko Kanu na Victor Ikpeba ndio wachezaji wa kwanza kutoka Nigeria kunyakua tuzo hiyo mtawalia miaka 1996 na 1997.

Banda alishinda tuzo ya mwanandinga bora kwa vipusa, akiisaidia klabu yake ya Orlando Pride ya Marekani, kutwaa taji ya Shield na pia ligi Kuu kando na kupachika mabao matatu kwa timu ya taifa ya Zambia kwenye Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.

Mlinda lango wa Afrika Kusini Ronwen Williams alitawazwa kipa bora wa mwaka na pia mchezaji bora wa mwaka kwa wanandinga wanaosakata soka barani Afrika.

Williams alipangua penati kadhaa kwa timu ya Afrika Kusini katika makala ya mwaka huu ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast, zikiwemo nne dhidi ya Cape Verde katika robo fainali, na kuiwezesha Bafana Bafana kumaliza ya tatu  AFCON.

Kipa huyo aliye na umri wa miaka 32 pia aliwasaidia Mamelodi Sundowns, kumaliza msimu uliopita wakifungwa idadi ndogo sana ya mabao, yakiwa 11.

Emerse Fae aliyeisaidia Ivory Coast kutwaa Kombe la AFCON akiwa kaimu kocha, alishinda tuzo ya kocha bora huku Lamia Boumehdi wa TP Mazembe, akiibuka kocha bora kwa wanawake.

Al Ahly ilishinda tuzo ya timu bora ya wanaume nayo  Mazembe iliyotwaa Ligi ya Mabingwa mwaka huu ikinyakua tuzo ya wanawake.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *