Meneja wa chapa wa kampuni ya East African Breweries Limited (EABL), Lilian Nyambura Mbugua, ambaye alitoweka kutoka nyumbani kwa familia yake huko Gikono, Kaunti ya Murang’a Disemba 23, 2024, amepatikana.
Katika taarifa ya Jumanne, Disemba 31, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Kusini, Gitonga Murungi, alithibitisha kwamba msichana huyo wa umri wa miaka 28 amepatikana akiwa hai na salama.
Kulingana na familia ya Mbugua, Lilian Nyambura alipatikana katika kituo cha kuuza mafuta huko Maragua, Kaunti ya Murang’a. Inaripotiwa kwamba alikuwa mdhaifu na amechanganyikiwa.
Siku aliyotoweka aliondoka nyumbani saa 11 jioni, akiwa amevaa kitambaa kichwani na champali kama mtu ambaye alikusudia kurudi haraka.
Aliiacha simu zake za mkononi, funguo za gari, kipakatalishi, funguo za nyumba, na vitambulisho.
Mjombake kwa jina George Njuguna alisema kwamba alitoka kama mtu aliyekuwa akienda kwa matembezi. Mamake alikuwa akijishughulisha nyuma ya nyumba na hakufikiria sana kuhusu hilo.
Familia yake ilihofia alipotoweka na kuripoti katika kituo cha polisi cha Gikono Disemba 24. kesi hiyo baadaye ilikabidhiwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huko Kenol.
Katika jitihada za kubaini alikokuwa, polisi walikumbana na changamoto kwani hakutoka na simu au gari, vitu ambavyo vingesaidia kufuatilia harakati zake.
Konstebo Patrick Maina wa Kituo cha Polisi cha Gikono alitaja uchunguzi huo kuwa mgumu sana.