Mwanamuziki wa Uganda Lil Pazo amevunja kimya chake kuhusu hatua ya tume ya mawasiliano ya Uganda, UCC, ya kupiga marufuku nyimbo zinazochukuliwa kuwa chafu zikiwemo zake.
Pazo amekashifu hatua hiyo akisema kwamba huenda ikasababishia wasanii matatizo ya kifedha kwani mashabiki wa muziki nchini Uganda hupendelea muziki wa burudani tu na wala sio wa mafundisho.
Kulingana naye, imekuwa vigumu kwa wasanii kufanikiwa na nyimbo zinazotilia maanani maadili kwa kiwango kikubwa.
Pazo ambaye amekuwa kwenye tasnia ya muziki nchini Uganda kwa muda, anasema amejaribu kuimba nyimbo zenye mafundisho na hazikupokelewa vyema na mashabiki ikilinganishwa na nyimbo za burudani zenye maneno yanayochukuliwa kuwa yanakiuka maadili.
Mapema mwaka huu, wimbo wake uitwao ‘Enkudi’ ulipendwa sana na vijana hata ingawa una maneno machafu. Wimbo huo anasema ulimpa kazi nyingi na akaweza kujimudu.
Mchujo ulitekelezwa hivi maajuzi na UCC ukilenga kuondoa nyimbo chafu kwenye vituo vya redio, runinga na hata majukwaa ya mitandaoni.
Lil Pazo anatambua nia njema ya mchujo huo lakini ametamaushwa na ukosefu wa usaidizi kwa wasanii. Alizungumzia ukosefu ya utekelezaji wa hakimiliki za muziki nchini Uganda hali inayowaacha wasanii katika hatari ya kupoteza pesa nyingi.
“Ninaelewa kile ambacho UCC inajaribu kufanya, lakini wanasahau kwamba wasanii wa Uganda ni fukara sana. Bila sheria nzuri za hakimiliki, wasanii wanategemea nyimbo zilizovuma kuchuma riziki.” alisema Lil Pazo.