Kindumbwendumbwe cha kuwania taji ya Ligi ya Mabingwa A frika kitaingia mechi za mzunguko wa tatu hatua ya makundi kati ya Jumamosi na Jumapili hii.
Viongozi wa kundi A, Al Hilal Omdurman kutoka Sudan, watalenga kudumisha rekodi ya asilimia mia moja watakapozuru Algiers kupambana na MC Alger, huku mshindi wa mchuano huo akiongoza kundi.
Katika mechi nyingine, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, iliyo na pointi moja, itawaalika Young Africans kutoka Tanzania ambao wamepoteza mechi mbili za ufunguzi.
Wanajeshi wa FAR Rabat kutoka Morocco wanaoongoza kundi B kwa alama nne watakuwa ugenini kwa Maniema ya Congo wakati Mamelodi Sundowns ikiwa nyumbani Afrika Kusini kuwaalika Raja Casablanca ya Morocco.
Stade Abdijan ya Ivory Coast watakuwa wageni wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mechi pekee ya kundi C.
Kundini D kivumbi kinatarajiwa Esperance ya Tunisia ikicheza nyumbani dhidi ya Pyramids ya Misri Jumamosi katika Derby ya Kaskazini mwa Afrika, timu zote zikiwa na alama 4.