Mechi za makundi katika kipute cha kuwania kombe la Ligi ya Mabingwa barani Afrika CAF, zitakamilika mwishoni mwa juma huku timu mbili za mwisho kufuzu kwa robo fainali zikitarajiwa kubainika.
Tayari vilabu sita vimefuzu kwa ribo fainali vikiwa:-Toupiza Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutoka kundi A,Asec Mimosas ya Ivory Coast kutoka kundi B,Petro Atletico de Luanda ya Angola ya kundi C na mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri na Yanga ya Tanzania katika kundi D.
Kundi D litakamilisha mechi zake Ijumaa,Ahly maarufu kama Red Devils wakiwa nyumbani Cairo, dhidi ya Young Africans ya Tanzania huku mshindi akiongoza kundi hilo kuanzia saa moja usiku.
Katika mkwangurano mwingine Medeama kutoka Ghana watakuwa ziarani Algiers dhidi ya CR Belouizdad.
Jumamosi wekundu wa Msimbazi Simba watakuwa nyumbani kwa Mkappa kuanzia saa kumi alasiri kuwapokea Jwaneng Galaxy kutoka Botswana katika kundi B, wakati viongozi Asec wakiwazuru Wydad Casablanca mjini Casablanca Morocco.
Simba ambao wanalenga kuwa timu ya pili ya Afrika Mashariki kutinga awamu ya nane bora msimu baada ya watani wao Yanga wanahitaji ushindi wowote ili kuafikia ruwaza hiyo.
Kwa upande wao Wydad ambao wanashikilia nafasi ya tatu kundini B, ni sharti waibwage Asec na kutarajia Simba watateleza dhidi ya Jwaneng.
Katika kundi A Jumamosi Mamelodi watawaalika Mazembe huku Pyramids ya Misri ikipambana na Nouadhibou ya Mauritania.
Katika kundi C,Esperance Tunis ya Tunisia itawaalika Al-Hilal Omdurman kutoka Sudan,wenyeji wanaokalia nafasi ya pili wakihitaji ushindi ili kufuzu kwa kwota fainali.
Waakilishi wa pili wa Tunisia Etoile Sahel watakuwa wageni wa Petro Atletico kutoka Angola Sahel wakihitaji ushindi na kutarajia watani wao Esperance watateleza ili kuingia mchujo wa nane bora.