Leslie Muturi ambaye ni mwanawe mwanasheria mkuu nchini Justin Muturi ameachiliwa huru. Inaripotiwa kwamba aliachiliwa jana Jumapili jioni baada ya saa kadhaa za kutoweka.
Baada ya maafisa wa polisi kukana kumkamata awali, sasa imebainika kwamba alikamatwa na maafisa wa usalama na kupelekwa kwenye afisi za kitengo cha kupambana na ugaidi katika eneo la Upper Hill, Nairobi.
Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje ndiye alifichua kwamba Leslie alikamatwa usiku wa Jumamosi, Juni 22, 2024 katika eneo moja la burudani kwenye barabara ya Dennis Pritt.
Alielezea kwamba Leslie mwenye umri wa miaka 40 alikuwa anaondoka kwenye sehemu hiyo ya burudani wakati gari lake lilifungiwa na gari jingine kisha akatolewa na kuelekezwa kwenye gari jingine na watu anaoamini walikuwa maafisa wa polisi.