Lalama zasheheni kufuatia uamuzi wa Rais Tinubu

Rais Tinubu alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Rivers jana kufuatia kuharibiwa kwa bomba kuu la mafuta.

Marion Bosire
2 Min Read
Bola Tinubu, Rais wa Nigeria

Watu wengi maarufu nchini Nigeria wamelalamikia hatua ya Rais wa nchi hiyo Bola Tinubu ya kutangaza hali ya hatari katika jimbo la Rivers.

Mwanamuziki Folarin Falana maarufu kama Falz amezungumzia suala hilo akisema kwamba hakuna sheria ambayo inamruhusu Rais kumsismamisha kazi Gavana.

Aligusia pia kuhusu jinsi Gavana huchaguliwa na anaweza tu kuondolewa madarakani kupitia bunge la jimbo hilo akishangaa iwapo kumetokea vita katika jimbo hilo au tishio lolote kwa serikali kuu.

Kulingana na katiba ya Nigeria, Rais anaweza kutangaza hali ya hatari iwapo kutatokea vita, hatari ya serikali kuingiliwa kinyume cha sheria, hali iliyokithiri ya watu kutofuata sheria, janga kubwa la kiasili au anapopokea ombi ya kufanya hivyo.

Mwigizaji na mwanasiasa Hilda Dokubo naye alimrushia maneno Rais Tinubu kuhusiana na hatua yake akisema, “Hali ya hatari kwa sababu kwa miaka miwili iliyopita tumekuwa na amani! Hali ya hatari kwa sababu unataka kunyakua moyo wa kiuchumi wa jimbo la Rivers! Hali ya hatari kwa sababu ya mwanaume mmoja!”

Dokubo alimalizia chapisho lake kwa Instagram akisema kwamba Rais anafaa tu kusema kwamba anataka kunyakua jimbo la Rivers.

Katika chapisho jingine, Dokubo alipendekeza kwamba kila mkazi wa jimbo la Rivers apatiwe nakala ya kitabu “Animal Farm” kilichoandikwa na George Orwell.

Jana Jumanne Machi 18, 2025 Rais Tinubu alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Rivers lenye utajiri mkubwa wa mafuta kutokana na kile alichokitaja kuwa uharibifu uliokithiri wa mambomba ya mafuta.

Katika hotuba kwenye runinga, Rais Tinubu alitangaza pia kwamba amewasimamisha kazi viongozi wote waliochaguliwa katika jimbo la Rivers ambao ni Gavana, Naibu Gavana na wanachama wa bunge la jimbo hilo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *