Lagat: Wanaofadhili uhalifu chuma chao ki motoni

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat (Kushoto) na Kamanda wa polisi eneo la Pwani Ali Nuno (Kulia).

Naibu Inspekta Jenerali wa Huduma ya Taifa ya Polisi Eliud Lagat, amewaonya wanaofadhili ghasia katika mikutano ya kisiasa, akisema watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza katika kaunti ya Mombasa alipokuwa akiwahutubia Maafisa Wakuu wa Polisi kutoka vitengo mbali mbali kote nchini, Lagat alisema asasi za usalama zimedokeza kuibuka kwa magenge ya wahalifu wakati wa mikusanyiko ya kisiasa.

Lagat alisema mkutano huo uliowaleta pamoja maafisa wakuu wa polisi utaangazia upya uendeshaji shughuli, kuimarisha mikakati na kushughulikia changamoto ibuka za kiusalama.

Aidha kulingana na Lagat, majadiliano katika mkutano huo, yataangazia utayari wa Uchaguzi Mkuu ujao, akisisitiza haja ya kudumisha usalama na amani wakati wa msimu wa kampeni na chaguzi zijazo.

Kadhalika, alisema maafisa wa usalama hawataruhusu shughuli za uhalifu, hususan zinazotekelezwa na wahalifu wanaojisingizia kuwa wahudumu wa Boda Boda.

Eneo la Pwani la taifa hili limeshuhudia ongezeko la visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na magenge ya wahuni, huku baadhi ya mikutano ya kisiasa katika sehemu kadhaa za nchini ikivurugwa na kusababisha maafa na majeruhi.

TAGGED:
Share This Article