Shirika la huduma kwa wanyama pori hapa nchini KWS, limewahimiza wakenya kupuuza habari zinazodokeza kuwa, shughuli za uchimbaji madini zinatekelezwa katika mbunga ya kitaifa ya Tsavo Mashariki, likisema habari hizo ni za kupotosha.
Shirika hilo lilifafanua hayo siku ya Jumatatu jioni, baada ya picha kusambazwa katika mitandao ya kijamii zikiashiria shughuli za uchimbaji madini zinatekelezwa katika mbuga hiyo.
“Tungependa kufafanua kwamba, picha ambazo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, sio za mbuga ya kitaifa ya Tsavo Mashariki, na kwamba hakuna shughuli zozote za uchimbaji madini zinaendelea,” ilisema taarifa kutoka shirika hilo.
Kulingana na KWS, picha hizo zinazoashiria kuna uchimbaji madini katika mbuga hiyo, zilipigwa kutoka mradi tofauti wa serikali katika kaunti jirani ya Tana River.
“Picha hizo ni za mpango wa unyunyiziaji mashamba maji wa Galana Kulalu, ulioko katika shamba la Galana na unaosimamiwa na unaosimamiwa na shirika la maendeleo ya kilimo ADC,” iliongeza taarifa hiyo.
Mradi wa Galana Kulalu unatekelezwa na serikali chini ya idara ya unyunyiziaji mashamba maji, kwa lengo la kuimarisha usalama wa chakula hapa nchini.