Ni asilimia 41 tu ya Wakenya wanaotaka Naibu Rais Rigathi Gachagua afurushwe kutoka wadhifa huo.
Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na kampun ya TIFA, asilimia 38 ya Wakenya waliohojiwa wanasema wanapinga Gachagua kuondolewa kwenye wadhifa huo.
Kulingana na kura hiyo ya maoni, asilimia 21 ya Wakenya ama hawakutoa maoni au hawakuwa na uhakika juu ya suala hilo.
Utafiti huo unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanaopinga kutimuliwa kwa Gachagua wanatokea eneo la Mlima Kenya ambayo ni ngome yake ya kisiasa.
Utafiti huo unaashiria kuwa asilimia 69 ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya wanapinga Naibu Rais kutimuliwa kwenye wadhifa huo huku asilimia 20 ya wakazi wakiunga mkono kufurushwa kwake. Ni asilimia 11 pekee ya wakazi ambao hawakuwa na uhakika juu suala hilo.
Katika maeneo mengine ya nchi, asilimia 47 ya waliohojiwa wameunga mkono kubanduliwa kwa Gachagua huku asilimia 28 wakipinga na asilimia 24 kutokuwa na uhakika.
Wanaotaka atimuliwe wanasema, miongoni mwa sababu zingine, kwamba Naibu Rais amekuwa akitoa matamshi ya chuki, utenda kazi wake umekuwa mbovu, wenye ufisadi na kwamba migawanyiko imeibuka kati yake na Rais.
Wanaopinga wanasema anashambuliwa bila sababu za msingi, utenda kazi wake ni mzuri na ni mtu mwaminifu, yeye na Rais William Ruto wanapaswa kufanya kazi pamoja kumaliza muhula wao na kwamba anapaswa kusamehewa na kupewa fursa nyingine.
Utafiti huo ulifanywa kati ya Oktoba 1-4, 2024 huku watu 1,892 wakihojiwa katika kaunti zote 47 kote nchini.