Asilimia 56 ya Wakenya wanaamini nchi hii imechukua mwelekeo mbaya.
Hii ni kulinganisha na asilimia 48 ya Wakenya waliokuwa na maoni sawia mwezi Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na kampuni ya TIFA Research kati ya Juni 24 na 30 ikiwahusisha watu 1,530, idadi ya wanaomini nchi imechukua mwelekeo mbaya iliongezeka kwa asimilia nane mwezi Juni ikilinganishwa na miezi mitatu iliyopita.
Asilimia 79 ya waliohojiwa walitaja kupanda kwa gharama ya maisha kuwa sababu kuu.
Kwa upande mwingine, asilimia 25 walisema nchi imechukua mwelekeo mzuri.
Idadi hiyo ilipungua kwa asilimia 12 ikilinganishwa na utafiti uliofanywa na kampuni hiyo mwezi Machi.
Asilimia 43.6 wanaunga mkono serikali ya Rais William Ruto na wanampa gredi ya C+ kutokana na uchapa kazi wake.
Asilimia 18.4 wanaunga mkono utendakazi wa upande wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga wakati asilimia 26.6 wakielezea kutounga mkono upande wowote.
Waliohojiwa walitaja kuzinduliwa kwa hazina ya Hustler na udhibiti wa bei ya mbolea kuwa baadhi ya mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza huku hali ngumu ya kiuchumi na kutotimiza ahadi za uchaguzi mkuu uliopita yakitajwa kuwa mapungufu ya utawala wa Kenya Kwanza.
Waliohojiwa walimtaja Waziri wa Ulinzi wa Taifa Kithure Kindiki kuwa bora katika utendakazi serikalini kwa asilimia 34 akifuatwa na Mawaziri Ezekiel Machogu wa Elimu kwa asilimia 7, Susan Nakhumicha wa Afya kwa asilimia 6, Ababu Namwamba wa Michezo kwa asilimia 3 na Kipchumba Murkomen wa Barabara na Uchukuzi kwa asilimia 2.