Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo nchini, KUPPET, kimeitaka Tume ya Kuwaajiri Walimu, TSC, kuchapisha majina ya watakaopandishwa vyeo.
Katika kikao na wanahabari jana katika afisi za chama hicho kaunti ya Nairobi, maafisa wa KUPPET wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Moses Nthurima, walitilia shaka zoezi la upandishaji vyeo wa walimu linaloendelea nchini.
Walidai zoezi hilo la kitaifa litakalokamilika wiki kadhaa zijazo halina uwazi, na kuishurutisha TSC kuchapisha majina ya wote watakaopandishwa ngazi.
TSC ilitangaza nafasi 1,000 za kupandishwa vyeo kwa walimu, idadi ambayo KUPPET inasema ni ndogo ikilinganishwa na walimu 11,000 ambao hawajapandishwa vyeo.
Walihoji pia uhalali wa zoezi hilo na mfumo unaotumika kugawanya nafasi hizo 1,000 kwa kaunti zote 47 kwa usawa bila kuzingatia kaunti zilizo na uhaba wa walimu.