Kunle Afolayan ambaye ni mwigizaji na mwandalizi wa filamu nchini Nigeria amepatana tena na kakake mdogo kwa jina Aremu Afolayan.
Mapatano kati ya wawili hao yalijiri katika hafla ya baada ya mazishi ya mama yao mzazi hatua ambayo Kunle anasema ilichochewa na mapenzi.
Katika video iliyosambazwa mitandaoni, Kunle anasikika akisema kwamba yeye sio tu kaka mkubwa wa Aremu bali pia ni babake kwani alimtunza.
Alifichua pia tofauti iliyopo katika umri wao akisema amemzidi miaka 10.
Video hiyo inaonyesha wawili hao wakiwa wamesimama bega kwa bega huku Kunle akimwekelea Aremu mkono kwenye bega na waliokuwepo wakashangilia.
Kabla ya hapo, kwenye mkusanyiko wa mazishi ya mama yao, Aremu ambaye pia ni mwigizaji, alibubujikwa na machozi huku akimwomba Kunle msamaha.
Aremu aliwahi kumchamba Kunle na ndugu zao wengine kwenye Instagram akigusia magumu waliyopitia walipokuwa wadogo.
Wakati akiomba msamaha, Aremu alimshukuru Kunle kwa kujengea marehemu mama yao nyumba kisha wakakumbatiana.