Kundi la Hamas limesema liko tayari kuachilia mateka 34 kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel, haya ni kulingana na shirika la habari la Reuters na lile la AFP.
Kundi la Wapalestina, linalotawala Ukanda wa Gaza, limeridhia kuachilia mateka hao kama sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa, huku AFP ikinukuu afisa mmoja wa Hamas ambaye hakutaka kutajwa jina.
Kubadilishana kwa mwanzo kutahusisha wanawake, watoto, wazee na wagonjwa wanaoshikiliwa Gaza.
Afisa huyo wa Hamas alisema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yatategemea Israel kukubaliana na kusitisha mapigano na kujiondoa Gaza.
Afisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema Jumapili kuwa Hamas haijatoa orodha ya mateka kwa ajili ya kuachiliwa.
Ripoti hizi zinajiri wakati mazungumzo ya kuafikia makubaliano ya kusitisha mapigano yanaendelea huko Qatar.
Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden, ambao unasimamia mazungumzo hayo, unatumai kupata mafanikio ya dakika za mwisho kabla ya Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kuapishwa Januari 20.
Ripoti zinaashiria kwamba bado kuna tofauti kubwa za kisiasa kati ya pande husika kwenye mazungumzo hayo na uamuzi sasa uko mikononi mwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Mazungumzo hayo yanatokea pia katika muktadha wa onyo la Trump kuhusu matokeo ya kutoafikiwa kwa makubaliano.
Trump alionya wiki chache zilizopita kwamba kama mapigano hayatakuwa yamesitishwa kufikia wakati atakapoapishwa, basi moto utazuka.
Israel iliendelea na mashambulizi Gaza Jumapili, ambapo jeshi lake lilikiri kushambulia zaidi ya malengo 100 ya “magaidi” katika ukanda huo kwa mwishoni mwa wiki.
Maafisa wa afya wa Gaza walisema mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya Wapalestina 100, wakiwemo watu watano katika nyumba kwenye kambi ya Nuseirat na watano katika kituo cha polisi huko Khan Younis.
Zaidi ya Wapalestina 45,800 wameuawa tangu Israel ilipoanzisha vita huko Gaza kwa kujibu mashambulizi ya Hamas dhidi ya nchi hiyo yaliyofanyika Oktoba 7, 2023.