Kukamatwa kwa Besigye kwachochea msururu wa shutuma

Martin Mwanje
2 Min Read
kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.

Viongozi mbalimbali nchini Kenya wameungana kulaani vikali ripoti za kukamatwa kwa Dkt. Kizza Besigye ambaye ni kiongozi wa upinzani nchini Uganda. 

Taarifa za kukamtwa kwa Besigye zilifichuliwa na mkewe Winnie Byanyima aliyedai mumewe alikamatwa akiwa jijini Nairobi mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua.

Serikali ya Kenya haijatoa taarifa yoyote juu ya madai hayo.

Ripoti zinaashiria kuwa Dkt. Besigye tayari amefikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Makindye ili kufunguliwa mashtaka.

Mashtaka yanayomkabili hayajabainika kufikia sasa.

“Nina wasiwasi mkubwa kwamba kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye ametoweka wakati akiwa ziarani jijini Nairobi. Hii ni hali nyeti inayohitaji kuchukuliwa kwa hatua mara moja,” amesema kiongozi wa upinzani nchini Kenya Kalonzo Musyoka.

“Natoa wito kwa mamlaka husika na taasisi za usalama kuchukua hatua za haraka na kubaini aliko Kizza Besigye na kumrejesha akiwa salama kwa familia yake.”

Matamshi sawia yametolewa na Mtandao wa Vuguvugu la Viongozi wa Upinzani barani Afrika, unaoongozwa na kinara wa chama cha Narc Kenya Martha Karua.

“Tunatoa wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa Dkt. Bessigye na kulaani vikali ukiukaji wa sheria ya manispaa, kikanda na kimataifa unaofanywa na taasisi za usalama,” ilisema taarifa kutoka kwa mtandao huo ambayo pia ilitiwa saini na viongozi kutoka nchi jirani za Burundi na Tanzania.

Mwanasheria Gitobu Imanyara pia amelaani vikali ripoti za kukamtwa kwa Dkt. Besigye akiwa jijini Nairobi akiitaka serikali ya Kenya kuelezea ni kwa namna gani ukamataji huo ulifanyika.

Dkt. Besigye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Yoweri Museveni na juhudi zake za kutaka kumbandua Rais huyo madarakani mara kadhaa zimegonga mwamba.

Share This Article