Chama cha wafanyakazi wa Nyumbani, Mikahawa, Hospitali na Shule, KUDHEIHA, kimemtaka Waziri wa Elimu Julius Ogamba kuingilia kati na kuwanusuru wafanyakazi wasaidizi katika shule za sekondari nchini takriban nusu milioni ambao wamepewa ilani za kusimamishwa kazi.
Katibu Mkuu wa KUDHEIHA Albert Njeru amemtaka waziri Ogamba, kuitisha kikao na chama hicho ili kujadili mwelekeo wa wafanyakazi hao badala ya kuwaachisha kazi.
Wafanyakazi hao walioajiriwa na halmashauri za usimamizi wa shule za sekondari (BOG), hususan waliokuwa wakihudumu katika kidato cha kwanza, watasimamishwa kazi kutokana na kutokuwepo kwa kidato cha kwanza mwaka huu.
Hii ni kufuatia kuanzishwa kwa mtaaala mpya wa elimu ya unilisi, CBC, ambao unaingia Gredi ya tisa mwaka huu.
Njeru amependekeza wafanyakazi hao kuhamishiwa katika shule za sekondari ya chini, JSS badala ya kusimamishwa kazi.
Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka wafanyakazi wote waliopewa ilani za kusimamishwa kazi kuwaarifu maafisa wa KUDHEIHA ili kutafuta suluhu.