KRA yaafikia lengo la shilingi trilioni moja la ushuru

Kiwango hicho kinaashiria ukuaji wa asilimia 4.3 ya kiwango cha ushuru uliokusanywa katika kipindi sawia mwaka 2023/2024 ambapo KRA ilikuwa imekusanya Trilioni 1.009.

Marion Bosire
2 Min Read

Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini Kenya, KRA imetangaza kwamba ilikusanya ushuru wa shilingi Trilioni 1.005 kufikia mwisho wa Novemba 2024.

Kiwango hicho kinaashiria ukuaji wa asilimia 4.3 ya kiwango cha ushuru uliokusanywa katika kipindi sawia mwaka 2023/2024 ambapo KRA ilikuwa imekusanya Trilioni 1.009.

Ukusanyaji huu unaonyesha matokeo mazuri katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka wa matumizi ya pesa za serikali wa 2024/2025 ambapo Trilioni 1.005 zimekusanywa kati ya mwezi Julai na Novemba 2024 ikilinganishwa na bilioni 963.746 zilizokusanywa kipindi sawia mwaka jana.

KRA hata hivyo imekumbana na changamoto kadhaa zinazotokana na sababu za kiuchumi ambazo zinahujumu ukusanyaji ushuru.

Changamoto hizo zinahusisha kupungua kwa mahitaji ya bidhaa na huduma kati ya wakenya kulingana na takwimu za hali ya sekta za viwanda na huduma.

Shughuli za kiuchumi zilionekana kupungua pakubwa katika kipindi hicho huku ukuaji wa sekta ya uagizaji bishaa ikishuhudia ukuaji wa asilimia moja tu.

Mipango ya serikali ya kupunguza matumizi imeathiri pia ukusanyaji ushuru hasa katika sekta zinazotegemea bidhaa zinazotozwa ushuru wa thamani yaani VAT.

Idara ya forodha hata hivyo imeonyesha ustahimilivu wa kiwango cha juu ambapo imekuwa ikizidi shilingi bilioni 70 kila mwezi tangu Agosti hadi Novemba 2024.

Kwa jumla mapato yaliyokusanywa katika idara ya forodha kwenye kipindi cha Julai hadi Novemba 2024 ni bilioni 359.571 ukuaji wa asilimia 5.9 ikilinganishwa na bilioni 339.678 zilizokusanywa kipindi sawia mwaka uliopita wa kiserikali.

Ushuru wa humu nchini pia uliongezeka ambapo ulikuwa bilioni 643.790 kati ya Julai na Novemba 2024, ukuaji wa asilimia 3.5 ikilinganishwa na bilioni 621.984 za mwaka uliopita wa kiserikali.

KRA sasa imejiwekea kiwango kipya cha malengo ya ukusanyaji ushuru ambacho ni Trilioni 2.704 katika mwaka wa kiserikali wa 2024/2025.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *