Kampuni ya umeme nchini KPLC imemulikwa kwa kile kinachotajwa kuwa kuacha nyaya za umeme zikining’inia kwa njia hatari kwa miaka miwili sasa katika kijiji cha Kimao huko Baringo Kusini kaunti ya Baringo.
Wakazi wanaohofia hatari inayowakodolea macho kutokana na hali hiyo karibu na shule ya msingi ya Kimao wanasema wamekuwa wakiripoti suala hilo kwa KPLC kwa miaka miwili sasa na hatua haijachukuliwa.
Wanalalamika pia kwamba eneo hilo limekuwa bila huduma ya umeme tangu nchi ilipojipatia uhuru na wanahisi kwamba wametengwa.
Mwanzoni walikuwa na matumaini ya kupata huduma za umeme lakini matumaini yao yalififia baada ya nguzo zilizowekwa kuliwa na mchwa huku mtambo wa Transformer ukiondolewa miaka miwili iliyopita.
Nyaya hizo sasa ni tishio kwa wakazi hasa watoto pamoja na mifugo wao.
Wanaogopa kwamba iwapo nyaya hizo zitaungana na nyaya nyingine zinazotoa umeme kwenye mtambo wa Transformer hadi kwa bwawa la Kimao ajali huenda zikashuhudiwa.
Kulingana nao iwapo hatua haitachukuliwa kabla ya ufunguzi wa shule kwa muhula wa tatu, basi watalazimika kuondoa nyaya hizo wenyewe na kuziuza kama vyuma kuu kuu.
Ombi lao kwa mbunge wao Charlse Kamuren na kwa kampuni ya KPLC ni kwamba nguzo za nyaya za umeme ziwekwe upya na waunganishiwe umeme.