Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Dawa Nchini, KPDA Dkt. Isaac Murichu, ameonya kuwa huenda Kenya ikakumbwa na upungufu wa dawa na ongezeko la bei kwa bidhaa hizo maalum endapo serikali haitaingilia kati kudhibiti hali.
Dkt. Murichu anaitaka serikali kuanza kudhibiti bei ya dawa na vifaa vya matibabu kinyume cha hali ilivyo kwa sasa ambapo wasambazaji wa kibinafsi wanaofanya biashara ndio wanaofanya maamuzi.
KPDA imekuwa na jukumu la kuagiza dawa tangu mwaka 2005 .
“Endapo serikali haitaanza kudhibiti bei ya dawa na vifaa vingine vya matibabu, itakuwa vigumu kwa raia wa kawaida kumudu ada ya dawa za matibabu, ”alisema Dkt. Murichu.
Kulingana na Dkt. Murichu, Kenya ni baadhi ya mataifa yaliyo na bei ghali ya dawa ikiwa kati ya asilimia 500 na 700, ikilinganishwa na masoko mengine kama Uingereza, Ujerumani, Marekani na India.
Mwenyekiti huyo wa KPDA amemtaka Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kuingilia kati kuwaokoa Wakenya dhidi ya madalali wa kibinafsi wanaongeza bei ya dawa kila uchao na jinsi wapendavyo, akiahidi kuwa wako tayari kumsaidia Waziri kudhibiti hali.