Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ameelezea wasiwasi kuhusu visa vinavyozidi kuripotiwa vya ufisadi na kuajiriwa kwa watu kwa misingi ya kujuana kifamilia na kirafiki katika kaunti mbalimbali nchini.
Koskei aliwataja watu walio na uhusiano wa karibu na wanasiasa walio na ushawishi mkubwa ambao wanadaiwa kujipatia pesa za umma kupitia kwa matumizi mabaya ya michakato ya kutoa zabuni, ununuzi wa bidhaa na kupitia mifumo ya kukusanya mapato.
Aidha, alitaja malipo yasiyofaa yanayotolewa na kaunti kugharimia miradi ambayo tayari imetekelezwa na serikali ya taifa.
Koskei alikuwa akiongea mjini Naivasha wakati wa mkutano unaoendelea kuhusu uhusiano baina ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.
Alisema kuwa serikali za kaunti zinawaajiri watu wasiofaa na kusababisha utoaji wa huduma duni.
Koskei alizishtumu serikali za kaunti kwa kutoa kipaumbele kwa pesa za matumizi ya mara kwa mara badala ya kuangazia maendeleo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC ya mwaka wa 2023 kuhusu ukaguzi wa maswala ya ukabila katika utumishi wa umma, zaidi ya asilimia 80 ya kazi nchini zinatawaliwa na makabila kumi.