Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ametoa onyo kali kwa maafisa wa manunuzi katika wizara na idara za serikali akiwataka kujiepusha na ufisadi.
Onyo lake linakuja siku chache baada ya serikali ya kaunti ya Kilifi kuwataka maafisa kadhaa wa manunuzi kwenda kwenye likizo ya kulipwa ya siku 90 kutokana na mienendo yao iliyosemekana kutatiza utoaji huduma.
Maafisa hao aidha walituhumiwa kwa kushawishi utoaji zabuni katika kaunti ya Kilifi.
Jijini Mombasa alikozungumza alipofungua kongamano la wakuu wa manunuzi na usimamizi wa mtungo wa usambazaji, Koskei alisema serikali ya Rais William Ruto imedhamiria kuandikisha upya mwelekeo wa historia ya nchi hii kwa kukabiliana vikali na zimwi la ufisadi.
Kulingana naye, vita vinavyoendelea dhidi ya uovu huo tayari vinazaa matunda.
“Nawatia moyo maafisa wa manunuzi kukataa ufisadi. Tunajua kinachofanyika katika kila taasisi. Tunachukua hatua haraka. Mnaweza mkaona taasisi zikiwachunguza washukiwa na baadhi wakipelekwa mahakamani. Ikiwa upo katika upande sahihi wa historia, hauna haja ya kuhofu,” alisema Koskei.
Mkuu huyo wa Utumishi wa Umma alitoa wito kwa maafisa wanaofanya kazi katika sekta za umma na binafsi kudhamiria kuhesabiwa katika kundi la wataalam wanaohakikisha manunuzi ni taaluma inayoheshimika.
“Hebu tukabiliane na ufisadi. Hebu tuwe mashujaa na hebu tuwe makamanda wa dhati wanaojaribu kuua ufisadi. Hii itasaidia kuchangia kwa ukuaji uchumi wa nchi hii, kubuni nafasi za ajira na kufanya nchi hii kuwa kitovu kinachowavutia wawekezaji.”