Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema serikali ya Rais William Ruto itaendelea kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa.
Kulingana naye, serikali itatekeleza mipango ya maendeleo katika sehemu zote za nchi bila kuzingatia jinsi watu walipiga kura katika maeneo tofauti wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Koskei alikuwa akizungumza kwenye hafla ya kutoa shukrani katika eneo la Rarieda, kaunti ya Siaya Ijumaa, ambapo alisisitiza kwamba kila Mkenya atafurahia huduma na fursa kwa njia sawa kutoka kwa serikali.
Alikuwa ameandamana na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo, makatibu wa wizara Dr. Belio Kipsang na Dr. Raymond Omollo pamoja na wabunge na viongozi wengine serikalini.
Aliongeza kuwa hatua ya serikali ya kuchagua kuhudumia kila Mkenya kwa usawa sio ya kushawishi yeyote huku akisihi watumishi wa umma wajitolee kazini kwani Wakenya lazima wanufaike kutokana na ushuru wao.
Mkuu huyo wa utumishi wa umma alionya watendakazi wa serikali dhidi ya ufisadi na kuwashauri wananchi dhidi ya matumizi ya pombe na mihadarati.
Waziri Owalo kwa upande wake aliomba wananchi wa eneo la Nyanza waunge mkono serikali ya Rais Ruto ambayo imejitolea kuleta maendeleo katika eneo hilo.
“Mtu asiwadanganye kwamba kutakuwa na mabadiliko serikalini hapa katikati. Hakuna mabadiliko hadi mwaka 2027 hata labda mwaka 2032,” alisema Owalo huku akisisitiza kwamba njia pekee ni kushirikiana na serikali iliyopo.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dr. Raymond Omollo aliwataka wawakilishi wa serikali kuu mashinani wahakikishe kwamba wanaendeleza sera za serikali kuu na kuzinadi kwa umma.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni wabunge Elisha Odhiambo, Gideon Ochanda, Felix Odiwuor (Jalang’o), mrakibu wa eneo la Nyanza Florence Mworoa na kamishna wa kaunti ya Siaya Jim Njoka kati ya wengine.