Waziri wa Mawasiliano na Uchumi Dijitali Eliud Owalo leo Jumatatu amezindua Kongamano la Ushirikiano wa Kidijitali, Utangamano na Maendeleo barani Afrika la mwaka 2024.
Kongamano hilo litakaloleta pamoja marais wa mataifa ya bara Afrika litazingatia mafanikio ya mpango wa Connected Kenya ulioanzishwa miaka 12 iliyopita chini ya usimamizi wa halmashauri ya teknolojia, habari na mawasiliano nchini.
Hafla hiyo imepangiwa kuandaliwa Aprili 2-5, 2024 ikilenga kufanikisha hatua ya kukumbatia mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano na kufungua fursa za biashara barani Afrika kupitia mkataba wa biashara huru unaozingatia uchumi wa kidijitali.
Akizungumza kwenye mkutano wa asubuhi kuhusu kuunganisha Kenya kidijitali, Waziri Owalo alithibitisha kwamba wizara yake inaunga mkono hafla hiyo na kuashiria kuwa uzinduzi huo ulifanyika kwa wakati unaofaa na wa kihistoria kwa ushirikiano wa kidijitali barani Afrika.
Waziri alisema mkutano huo utatoa fursa kwa bara Afrika kujifunza tasnia ya teknolojia na kukumbatia hali bora zaidi katika ukuaji wa teknolojia.
Waziri Owalo alibainisha kuwa kwa kufuata yaliyojadiliwa kwenye makongamano ya awali kuhusu kushirikiana kiteknolojia, sekta ya kibinafsi na ya umma, kupitia ushirikiano huo, imeweza kuweka kikamilifu huduma 9,700 za serikali mtandaoni.
Alisema pia kwamba wizara yake inatoa mafunzo kwa vijana kupitia mpango wa Jitume na Ajira na itaongeza malengo ya kongamano la ushirikiano wa Afrika kidijitali la mwaka 2024.
Kwa upande wake, Prof Kisiang’ani ambaye ni katibu katika wizara hiyo anayehusika na masuala ya utangazaji na mawasiliano, amewahakikishia wadau kuwa serikali imejizatiti kuendeleza mawasiliano kupitia ushirikiano na sekta ya binafsi ili kuimarisha maendeleo.