Kongamano la ufadhili wa mifumo ya kilimo na chakula Afrika lazinduliwa

Katibu wa idara ya kilimo Kiprono Ronoh alizindua kongamano hilo leo jijini Nairobi akisisitiza jukumu muhimu la kilimo katika uchumi wa Kenya.

Marion Bosire
3 Min Read

Awamu ya pili ya kongamano kuhusu ufadhili endelevu wa mifumo ya kilimo na chakula barani Afrika imeanza rasmi leo jijini Nairobi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo, katibu wa idara ya kilimo Kiprono Ronoh alisisitiza kuhusu jukumu muhimu la kilimo katika uchumi wa taifa la Kenya, ambapo kinachangia asilimia 20 ya pato jumla la taifa na kuajiri asilimia 40 ya wakenya.

Alisema wakulima hasa wale wadogo wanahitaji ufadhili wa kuweza kununua pembejeo, kukodisha masgamba, kununua mifugo na kutimiza mahitaji mengine.

Katibu huyo alisema kwamba kongamano hili ni jukwaa muhimu la kuangazia suluhisho bunifu za ufadhili kwa lengo la kuhakikisha uendelevu wa mifumo ya kilimo na chakula kote barani Afrika.

“Ni fursa ya kuunda mustakabali wa mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika.” alisema Rono.

Rono aliongeza kwamba kuambatana na ajenda ya serikali, mipango ya kilimo imepatiwa kipaumbele kulingana na mkakati wa serikali wa kuwezesha watu wa chini almaarufu Bottom-Up Economic Agenda (BETA.

Mpango huo kulingana naye unalenga kuafikia uwepo wa chakula, kupunguza uagizaji kutoka nje na kuimarisha mauzo ya nje ya nchi.

Alielezea kwamba mwaka wa serikali wa 2025/2016, serikali imetenga shilingi bilioni 77.7 kwa shughuli za kilimo, hatua kubwa katika kuongeza uwekezaji wa kuimarisha uzalishaji, kupunguza hasara baada ya mavuno na kutoa fursa zaidi za ajira.

Katibu Rono alisema pia kwamba Kenya imejilainisha sambaba na mipango ya bara Afrika kama mpango wa pamoja wa maendeleo ya kilimo – CAADP na tamko la Malabo.

Kulingana naye mipango hiyo imeimarisha mbinu endelevu, uundaji wa viwanda vya bidhaa za kilimo na biashara ya kimaeneo, na kuiweka mbele katika mikakati ya kitaifa na kibara.

Ronoh alisisitiza umuhimu wa kuhusisha sekta ya kibinafsi katika kubadili mifumo ya kilimo na chakula, akiangazia mafanikio ya awamu ya kwanza ya kongamano la ufadhili endelevu wa mifumo ya kilimo na chakula barani Afrika mwaka 2024.

Huku ufadhili wa ulimwengu wa sekta muhimu ukiendelea kupungua, Ronoh alisema kwambaserikali inatafuta suluhisho bunifu la ufadhili.

Alikumbusha wanaohudhuria kwamba kongamano hilo sio tu la ufadhili bali pia linalenga kutathmini jinsi ya kuwekeza katika kilimo na hivyo kuunda mifumo ya chakula ambayo ni stahimilivu, endelevu na jumuishi.

Katibu huyo alihimiza juhudi za pamoja za wadau wote katika kushughulikia changamoto zinazokumba sekta ya kilimo.

Website |  + posts
Share This Article