Umoja wa Afrika (AU) ulimaliza kongamano lake maalum tarehe 11 Januari 2025, kwa tamko la kihistoria lililolenga kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula Barani Afrika kufikia mwaka 2035.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Kampala nchini Uganda, kilikutanisha viongozi wa nchi na serikali, waliothibitisha kujitolea kwao kwa Mpango wa Maendeleo ya Kilimo wa Afrika (CAADP) na kuahidi kushughulikia changamoto za usalama wa chakula na uendelevu katika bara hili.
Kiini cha Tamko la Kampala CAADP ni ahadi ya kuongeza uzalishaji wa kilimo na chakula kwa asilimia 45 ifikapo 2035, kwa kuzingatia mbinu endelevu za kilimo na viwanda vya kilimo.
Viongozi hao pia walikubaliana kupunguza hasara za baada ya mavuno kwa kiwango cha asilimia 50 na kuongeza mara tatu biashara ya ndani ya Afrika ya bidhaa za kilimo na chakula, wakizingatia malengo ya Eneo la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA).
Aidha, walisisitiza umuhimu wa teknolojia, ubunifu, na ushirikiano wa kanda katika kujenga mifumo ya kilimo na chakula inayostahimili na inayo jumuisha.
Tamko hilo linajumuisha malengo ya kipevu ya kuongeza uwekezaji, likilenga kukusanya dola bilioni 100 kutoka kwa sekta za umma na binafsi ifikapo 2035.
Uwekezaji huu utaangazia kuboresha miundombinu, kuendeleza utafiti wa kilimo, na kuhakikisha ushiriki wa wanawake, vijana, na makundi yaliyotengwa katika minyororo ya thamani ya kilimo na chakula.
Kwa kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanatishia uzalishaji wa kilimo, kikao hicho kilisisitiza umuhimu wa kujenga ustahimilivu, ikiwa ni pamoja na usimamizi endelevu wa ardhi, mbinu za kilimo zinazozingatia tabia nchi, na uhifadhi wa maji.
Ahadi ya usalama wa chakula na lishe pia ni kipengele muhimu katika mpango huu, ikiwa na lengo la kufikia sifuri ya njaa na kupunguza utapiamlo katika bara hili.
Viongozi wa Umoja wa Afrika walitoa wito kwa hatua zinazoratibiwa katika ngazi za kitaifa, kanda, na bara nzima ili kutekeleza ahadi hizi, wakisisitiza umuhimu wa utawala bora, uwajibikaji, na ukuaji unaojumuisha.
Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa CAADP, wa mwaka 2026 hadi 2035, utatoa mwelekeo wa mabadiliko ya mifumo ya kilimo na chakula ya Afrika katika miaka ijayo.
Ramani hii ya mbinu ya kijasiri kwa ajili ya mifumo ya kilimo na chakula ya Afrika ni hatua muhimu katik kuhakikisha usalama wa chakula, kuboresha lishe, na kukuza ukuaji wa kiuchumi endelevu katika bara hili.