Chama cha walimu KNUT kimepinga pendekezo la jopo lililobuniwa na rais kumshauri kuhusu mageuzi katika sekta ya elimu la kuwashusha vyeo walimu wakuu wa shule za msingi wasio na shahada.
KNUT badala yake inapendekeza kwamba walimu wakuu wa shule za msingi ambao hawana shahada wapatiwe muda wasome ili wazipate. Kulingana na pendekezo hilo la jopo la rais la mageuzi katika sekta ya elimu, walimu hao wataongoza shule ambazo zina secondari za chini au Junior Secondary hadi mwezi Disemba mwaka huu.
Katibu mkuu wa KNUT Collins Oyuu alisema wanaunga mkono mapendekezo kadhaa ya jopo hilo kuhusu mageuzi katika sekta ya elimu ambayo bado hayajaratibiwa na rais ili kuanza kutekelezwa lakini wanapinga hilo tu la kushusha walimu vyeo.
Oyuu alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa baraza la KNUT eneo la pwani katika shule ya msingi ya Ronald Ngala huko Mombasa ambapo alisema wengi kati ya walimu wakuu wa shule za msingi za umma wana vyeti vya shahada na waliosalia wanaweza kuvipata.
Jopo la rais la mageuzi katika sekta ya elimu linapendekeza kwamba shule za chekechea, msingi na sekondari ya chini ziwe kwenye eneo moja chini ya usimamizi wa mwalimu mmoja mkuu. Tume ya kuajiri walimu nchini TSC itatoa mwelekeo kuhusu walimu wandamizi watakaofanya kazi chini ya walimu wakuu ili kuongoza vitengo hivyo vitatu.