KMPDU yataka madaktari wakufunzi kuanza mafunzo katikati ya Juni

Martin Mwanje
1 Min Read

Chama cha Madaktari nchini, KMPDU sasa kinapendekeza madaktari wakufunzi kuanza mafunzo yao katikati ya mwezi huu. 

Mpango wa utoaji mafunzo kwa madaktari hao ulisitishwa baada ya utata kuzuka kuhusiana na malipo ya mshahara wa shilingi elfu 70 yaliyopendekezwa na serikali.

KMPDU inataka madaktari wakufunzi kulipwa shilingi 206,000 kama ilivyokuwa kwa wenzao waliotangulia kwa mujibu wa mkataba wa maelewano, CBA wa mwaka 2017.

“Ikizingatiwa madaktari wakufunzi wa sasa watakamilisha uanagenzi wao mwezi Julai, 2024, tunapendekeza kutumwa kwa kundi lijalo la madaktari wakufunzi kufanywa katikati ya mwezi Juni hata wakati tukiendelea kutafuta masharti ya kazi yanayokubalika ndani na nje ya mahakama,” ilisema KMPDU katika taarifa baada ya kukutana maafisa wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Katibu Mary Muthoni.

“Hii itahakikisha kuwa hawapotezi muda huku pia Wakenya wakiendelea kufurahia huduma zisizotatizwa.”

KMPDU haikubainisha malipo yatakayotolewa kwa madaktari wakufunzi hao ikiwa watatumwa kuhudumu katika hospitali mbalimbali za umma kuanzia katikati ya mwezi huu ikizingatiwa serikali inataka walipwe shilingi elfu 70.

Kwa mujibu wa KMPDU, wakati wa mkutano huo, ilikubaliwa kuwa madaktari wakufunzi wa sasa watalipwa malimbikizi ya mshahara wao wa mwezi Aprili pamoja na mshahara wao wa mwezi Juni.

Share This Article