Kizza Besigye apelekwa kliniki huko Bugolobi

Familia ya Besigye ilitangaza kwamba ilitakiwa kutuma daktari wake alikozuiliwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge mmoja wa Uganda kwa jina Francis Mwijukye alifichua jana kwamba Kizza Besigye ambaye ni kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda, alikimbizwa kwenye kliniki moja huko Bugolobi jana.

Mwakilishi huyo wa kaunti ya Buhweju bungeni alifafanua kwamba Besigye aliyekuwa akitumia kiti cha magurudumu alipelekwa kwenye kliniki moja iliyo kwenye orofa ya tatu ya jumba la kibiashara la Bugolobi village Mall.

Awali, familia ya Besigye ilikuwa imeibua wasiwasi baada ya kupokea ujumbe fulani kutoka kwa huduma ya magereza ya Uganda. Usimamizi huo wa magereza uliomba familia hiyo itume daktari wa kibinafsi wa Besigye.

Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya ripoti kuibuka kwamba Besigye alikuwa amenyimwa haki ya kupata huduma za matibabu akiwa kizuizini.

Wakwe zake Besigye walihutubia wanahabari Jumapili ambapo walifichua hayo, katika taarifa iliyotiwa saini na ndugu za mkewe Besigye Winnie Byanyima ambao ni Edith, Olivia, Martha, Anthony na Abraham.

“Sisi familia ya Besigye, tunatoa ujumbe huu tukiwa na huzuni kwa sababu ya jamaa wetu aliyetekwa, akaletwa hapa na kuzuiliwa kinyume cha sheria.” alisema Edith Byanyima.

Walishangaa ni kwa nini waliombwa watume daktari na usimamizi ule ule uliomnyima mwenzao haki ya kupata huduma za matibabu.

Walidhihirisha woga wao kwamba huenda hali ya kiafya ya mpendwa wao imedorora ndiposa wakaitishwa daktari.

Waliahidi kumwajibisha kiongozi wa taifa la Uganda Yoweri Museveni, kwa lolote litakalomfika Besigye.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *