Kizaazaa kilishuhudiwa katika mahakama ya kijeshi ya Makindye nchini Uganda wakati kundi fulani la mawakili lilizuiwa kuingia humo.
Mawakili hao waliofika kwa ajili ya kesi dhidi ya Kizza Besigye na msaidizi wake Sheikh Obeid Lutale, walisikika wakipaaza sauti zao wakitaka lango lililokuwa limelindwa na polisi lifunguliwe.
Besigye na Lutale wameshtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama na kumiliki bunduki kinyume cha sheria, baada yao kutekwa nyara jijini nairobi, Novemba, 2024.
Wanawakikilishwa na mawakili zaidi ya 40, akiwemo wakili martha Karua wa Kenya.
Kulingana na vyombo vya habari, walinzi katika mahakama hiyo walikuwa wamepatiwa orodha ya mawakili wanaoruhusiwa kuingia humo lakini wakaja wengi.
Mmoja wa mawakili hao kwa jina Eron Kiiza anaripotiwa kukamatwa na polisi wakati wa kizaazaa hicho baada ya kujibizana na walinzi waliomzuia kuingia mahakamani.
Akizungumza mbele ya mahakama, Karua ambaye anaongoza kundi la mawakili wa Besigye alisema kutokuwepo kwa wakili Eron Kiiza mahakamani ni hujuma.
Alilaumu mahakama akisema kwamba inaonekana ilikuwa na mpango wa kumzuia wakili Kiiza asiingie mahakamani akiongeza kusema kwamba alidhulumiwa kabla ya kuchukuliwa na polisi.
Karua hatimaye alipatiwa kibali cha muda cha kuhudumu kama wakili nchini Uganda ili aweze kuwakilisha mteja wake Kizza Besigye mahakamani.