Kiwanda cha uzalishaji wa mtindi chazinduliwa Kirinyaga

Martin Mwanje
2 Min Read

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika eneo la Gichugu, kaunti Kirinyaga wana kila sababu ya kutabasamu baada ya mojawapo wa vyama vyao vya ushirika kuzindua kiwanda cha kuzalisha mtindi.

Kiwanda hicho cha Chama cha Ushirika cha Rung’eto kinapatikana wadi ya Ngariama katika kaunti ndogo ya Gichugu.

Kilizinduliwa kwa usaidizi wa serikali ya kaunti ya Kirinyaga inayoongozwa na Gavana Anne Waiguru kupitia mpango wa uwezeshaji wa Wezesha.

Serikali ya kaunti imeweka vifaa vya kutengeneza mtindi katika kiwanda hicho.

Vifaa hivyo vina uwezo wa kutengeneza hadi lita 200 za mtindi kwa saa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa kaunti hiyo Jackline Njogu alisema kiwanda hicho ni sehemu ya mpango wa Gavana Waiguru kuongeza mapato ya wakulima kupitia kuongezea maziwa thamani.

Joyce Wanjiku, mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Rung’eto alipongeza msaada ambao umetolewa kwa muda mrefu kwa chama hicho ikiwa ni pamoja na kukikabidhi vifaa muhimu vinavyohitajika.

Aliongeza kuwa uzalishaji wa mtindi siyo tu kwamba utawaongezea wakulima mapato bali pia utakipa chama hicho utambulisho wa kipekee.

Kwa upande wake, Tabitha Nyaga ambaye ni mwanachama wa muda mrefu wa chama hicho alisema amefurahia mno kushuhudia kuzinduliwa kwa bidhaa mpya ya mtindi katika eneo hilo.

Vyama vingine kama vile Kirima, Pondago, New Ngariama, Rukingo na Kirinyaga Dairy tayari vimenufaika na mipango ya kufufua sekta ya maziwa katika kaunti hiyo.

Kaunti ya Kirinyaga ina takriban ng’ombe wa maziwa 90,000 wanaozalisha wastani wa lita milioni 65.3 kwa mwaka.

 

 

Share This Article