Kituo cha masomo ya kupambana na ufisadi Afrika kuanzishwa Kenya

Martin Mwanje
1 Min Read

Kenya imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Masomo ya Kupambana na Ufisadi na Utafiti barani Afrika. 

Kituo hicho kitaanzishwa na Umoja wa Mamlaka za Kupambana na Ufisadi barani humo, AAACA.

Kwa mujibu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini, EACC, uamuzi huo uliafikiwa kupitia azimio la AAACA wakati wa mkutano wake usiokuwa wa kawaida uliofanywa Januari 10, 2024.

“Kituo hicho kitawezesha kufanyika kwa masomo na utafiti ambao utaimarisha uongozi bora na jitihada za kupambana na ufisadi barani Afrika,” inasema EACC katika taarifa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak amefurahia uamuzi wa AAACA akisema kituo hicho kitatekeleza wajibu muhimu katika kuwezesha uendelezaji na uwianishaji wa mikakati ya kuzuia, kutambua, kuchunguza na kudhibiti ufisadi na makosa yanayohusiana na uovu huo barani Afrika.

Azimio la Baraza Kuu la AAACA linatambua jitihada zinazofanywa na Kenya kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa ya kupambana na ufisadi ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo ya kukabiliana na ufisadi.

AAACA ilianzishwa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Afrika, AU ili kukuza utekelezaji mwafaka wa mkataba wa umoja huo wa Kuzuia na Kupambana na Ufisadi na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ufisadi, mikataba ambayo Kenya imeitia saini.

Share This Article