Chuo Kikuu cha Kenya Methodist almaarufu KeMU kinapanga kuanzisha kituo cha matibabu ya matatizo ya akili kwa jina “Global Salama centre of mental health and psychology.” Kitaanzisha kituo hicho kwa ushirikiano na vyuo vikuu vya Makerere, Harvard, Kabare, McLean Medical School, Umma, Kampala, USIU, Meru, Karatina na Kisii katika bewa kuu la Meru.
Akizungumza baada ya kongamano la siku mbili kuhusu afya ya akili lililofanyika katika Chuo Kikuu cha KeMU, Prof. Edward Bantu ambaye ni mhadhiri wa saikolojia alisema kituo hicho kitasaidia kutoa matibabu kwa walioathirika na kusaidia pia kutathmini afya ya akili kwa watu kabla ya kuwaajiri.
Kitatumiwa pia kutoa huduma ya kwanza kwa walio na matatizo ya kiakili na hivyo kupima mapendeleo yao katika utaalamu wa kikazi na uwezo wa kikazi.
Bantu alisema kituo hicho pia kitatoa uhamasisho kuhusu uwepo wa uwezo wa kiasili ndani ya kila mtu utakaosaidia kujua taaluma wanazopenda ili wawekwe wanakostahili kikazi.
Wanaosomea saikolojia pia wataweza kutumia kituo hicho kupata uzoefu wa kazi unaohitajika kabla ya kufuzu.
Askofu Douglas Nchebere anayesimamia masomo ya theolojia na ushauri nasaha katika chuo cha KeMU alisema kongamano hilo pamoja na wazo la kujenga kituo cha matibabu ya matatizo ya kiakili ni muhimu hasa katika kusimamia matatizo ya kiakili baada ya mauaji ya “Shakahola” ambapo watu wengi walipoteza maisha kwa kupotoshwa na kiongozi wa dini.