Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amefungua rasmi kitengo cha matibabu ya macho katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki jijini Nairobi.
Gavana Sakaja alisema kitengo hicho kilichofunguliwa jana Jumatatu, kitaimarisha huduma za matibabu ya macho jijini Nairobi, ikizingatiwa kuwa hospitali nyingi za macho hapa nchini na kanda ya Afrika Mashariki, zinamilikiwa na watu binafsi.
Sakaja aliwashauri wakazi wa Nairobi kuwahimiza marafiki na jamaa zao walio na matatizo ya macho, kupokea matibabu katika hospitali hiyo kwa bei nafuu.
Kulingana na Gavana huyo, hospitali hiyo ina vitanda 28, vyumba viwili vya upasuaji, kiwanda kidogo cha utengezaji wa miwani na itasimamiwa na wataalam wa macho.
Mkurugenzi wa hospitali ya Mama Lucy Kibaki Benard Gituma alitangaza kuwa hospitali hiyo sasa ina uwezo wa kufanya upasuaji wa macho kupitia wataalam wa upasuaji walio na mafunzo ya hali ya juu.
Gituma alisema mgonjwa wa umri wa chini zaidi kufanyiwa upasuaji ni mtoto wa umri wa miaka minne, na wa umri wa juu zaidi alikuwa na umri wa miaka 89.