Kipyegon na Moraa kukitifua Athlos leo katika fungakazi

Dismas Otuke
2 Min Read
Faith Kipyegon

Bingwa mara tatu wa Olimpiki katika mita 1,500 Faith Kipyegon na bingwa wa dunia katika mita 800 Mary Moraa watashiriki makala ya kwanza ya mbio za Athlos NYC, zitakazoandaliwa leo, Septemba 26 mjini New York nchini Marekani.

Shindano hilo ambalo ni la wanawake pekee litakuwa la mwisho kwa Kipyegon na Moraa mwaka huu katika mbio za uwanjani.

Kipyegon na Moraa wanashiriki mbio hizo wakiwa roho juu baada ya kutwaa ubingwa wa Diamond League katika mkondo wa mwisho wa Brussels, Ubelgiji.

Susan Ejore aliyeshiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwezi uliopita pia atatimka mbio za mita 1,500.

Kwa upande wake, Ejore ambaye ni Mkenya anayeishi nchini Marekani pia anajivunia kushiriki michezo ya Olimpiki mwezi jana nchini Ufaransa kwa mara ya kwanza.

Kipyegon ambaye ni mshikilizi wa rekodi za Dunia katika mita 1,500 na maili 1 atatashiriki mita 1,500 akishindana na mshikilizi wa rekodi ya Dunia katika mita 5,000 Gudaf Tsegay wa Ethiopia na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mita 1,500 Deribe Welteji kutoka Ethiopia.

Wapinzani wengine ni Katie Snowden wa Uingereza, Cory MCgee wa Marekani na Susan Ejore wa Kenya.

Moraa atatimka mita 800 pamoja na Natoya Goule Toppin wa Jamaica, bingwa wa zamani wa dunia Halimah Nakaayi wa Uganda, Nia Akins wa Marekani, Addy Weiley wa Marekani na bingwa wa Dunia wa mashindano ya ukumbini Tsige Duguma kutoka Ethiopia.

Mbio hizo pia zitawashirikisha mabingwa wa Olimpiki Gabby Thomas na Marielaidy Paulinho wa Jamhuri ya Dominika, watakaoshiriki mita 200 na 400 mtawalia.

Mashindano hayo yanaandaliwa na Alexis Kerry Ohanian, mumewe bingwa mara 23 wa mashindano ya Grand Slam katika mchezo wa tenisi Serena Williams wa Marekani.

Mshindi wa kila fani atatuzwa shilingi milioni 7.6 za Kenya, ambayo ni maradufu ya zawadi ya pesa wanazotuzwa washindi wa Diamond League.

Share This Article