Mabingwa wa Olimpiki Faith Kipyegon na Beatrice Chebet walipokea tuzo ya Academy of Achievement katika dhifa inayofahamika kama Dinner of the Golden Plate. Dhifa hiyo iliandaliwa mjini New York nchini Marekani jana Jumapili usiku.
Kipyegon alituzwa baada ya kutwaa dhahabu ya tatu ya Olimpiki katika mbio za mita 1,500 mjini Paris, Ufaransa mwezi jana na pia kushinda fedha katika mita 5,000.
Kwa upande wake, Chebet alitwaa dhahabu mbili za mita 5,000 na 10,000 katika michezo hiyo ya Olimpiki, akiwa Mkenya wa kwanza kuafikia matokeo hayo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais William Ruto ambaye pia yuko mjini New York kuhudhuria Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).