Bingwa Dunia na Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon, anatafungua msimu wake wa mwaka huu katika mashindano ya Shanghai Diamond League nchini Uchina, Mei 16.
Kipyegon atatimka mbio za mita 5,000 katika mkondo huo wa kwanza wa Diamond League,kuashiria azma yake ya kutaka kuhamia mbio za barabarani.
Mwanariadha huyo aliye na umri wa miaka 32, alishinda dhahabu ya Dunia katika mbio za mita 5,000 mwaka 2023 mjini Budapest ,na kushinda medali ya fedha katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2024, na kufuatia na fedha nyingine mwaka jana mjini Tokyo, katika mashindano ya Dunia ya fani hiyo ya mizunguko 12 unusu.
Kipyegon anaorodheshwa wa nne bora katika mita 5,000, akijivunia muda wa dakika 14 sekunde 5.20.
Hata hivyo, Kipyegon anatarajiwa kushiriki fani ya 1,500 kwenye makala ya kwanza ya mashindano ya Ultimate, yatakayofanyika mjini Budapest kati ya Septemba 11 na 13 mwaka huu.