Bingwa mara tatu wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon alihitimisha msimu wake kwa ushindi wa makala ya kwanza ya mbio za Athlos NYC nchini Marekani mapema Ijumaa.
Kipyegon ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia aliziparakasa mbio za mita 1,500 kwa muda wa dakika 4 sekunde 4.79,akifuatwa na Diribe Welteji wa Ethiopia kwa dakika 4 sekunde 5.58 ,huku Susan Ejore wa Kenya akimaliza wa tatu kwa dakika 4 sekunde 6.25 .
Mary Moraa alimaliza wa pili katika mita 800 kwa dakika 1 sekunde 58.5, nyuma ya Tsige Duguma wa Ethiopia aliyeibuka mshindi kwa dakika 1 sekunde 57.43, huku Natoya Goule-Toppin wa Jamaica akimaliza wa tatu.
Kipyegon alituzwa shilingi milioni 7.6 kwa ushindi huo, huku Moraa akitia mkobani shilingi milioni 3.1 naye Ejore akatunukiwa shilingi milioni 1.27.
Mbio hizo ziliandaliwa na Alexis Ohanian,mumewe mshindi mara 23 wa tuzo ya Grand slam katika Tennis Serena Williams, ndizo mbio zenye kiwango kikubwa cha pesa na ziliwashirikisha wanawake pekee.