Makala ya 34 ya kipute cha kwuania kombe la AFCON nchini Ivory Coast yataingia siku ya nne kwa mechi tatu,moja ya kundi D na mbili za kundi E.
Stallions ya Burkina Faso watafungua ratiba ya siku kwa kukabiliana na Mauritania almaarufu Simba wa chinguetti, kuanzia saa kumi na moja jioni katika mechi ya kundi D
ugani de Paix mjini Bouaké.
Itakuwa mara ya tano kwa Burkinabe na Mauritania kuchuana mechi moja ikiishia sare na Burkina Faso wakishinda tatu.
Baadaye saa mbili usiku kundi E litaanza mechi zake,Tai wa Tunisia ukipenda Carthage Eagles watakwangurana na Brave Warriors kutoka Namibia katika uchanjaa wa
Amadou Gon Coulibaly Korhogo.
Namibia wanashiriki fainali za AFCON kwa mara ya nne huku Tunisia wakiwinda kombe la kwanza tangu mwaka 2004 wakiwa wenyeji.
Mechi ya pili ya kundi E itaanza saa tano usiku Tai wa Mali wakipimana ubabe na Bafana Bafana ya Afrika Kusini uwanjani Korhogo.
Afrika Kusini wameshinda mechi mbili ,mbili kuishia sare na Mali wakaibuka kidedea mara moja.