Kipsang’: Usalama umeimarishwa katika kipindi cha mitihani ya KCSE

Tom Mathinji
1 Min Read

Katibu katika idara ya elimu ya msingi Dkt. Belio Kipsang’, amewahakikishia watahiniwa kote nchini usalama wao, wanapofanya mtihani wa kidato cha nne KCSE.

Kulingana na Dkt. Kipsang’, warakibu wa maeneo walichukua hatua dhabiti za kiusalama, na kwamba mitihani hiyo ilianza kote nchini bila hitilafu zozote.

“Hata katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto kama vile Kaskazini mwa nchi, mitihani hiyo ilianza katika mazingira mazuri kwa wanafunzi wetu,” alisema Kipsang’.

“Tunawashukuru wenzetu katika wizara ya usalama wa taifa kwa kuhakikisha usalama katika eneo hilo na kufanikisha usambazaji wa mitihani,” aliongeza katibu huyo.

Katibu huyo alisema kuwa serikali imejitolea kupitia kundi la asasi mbali mbali kuhakikisha uadilifu wa mitihani hiyo.

“Tutaendelea kutumia kundi la asasi mbali mbali kwa sababu kila mmoja ana uwezo maalum. Kundi hilo linajumuisha maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, kufanikisha uchunguzi, maafisa wa polisi kutoa ulinzi, walimu kuhakikisha utaalam unatekelezwa na maafisa wa nyanjani kuwapiga jeki walimu,” alisema Kipsang.

Awamu ya pili ya mitihani ya KCSE, ilianza leo kote nchini kwa somo la kiingereza.

Website |  + posts
Share This Article