Kipkoech na Chepkwemoi watwaa fedha na shaba Peru

Dismas Otuke
3 Min Read

Denis Kipkoech na Diana Chepkwemoi waliishindia Kenya nishani za fedha na shaba katika siku ya tatu, ya mashindano ya Riadha Ulimwengni kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mjini Lima Peru mapema Ijumaa.

Kipkoech alimaliza wa pili kwenye fainali ya mita 3,000,  akiziparakasa kwa dakika 8 sekunde 20.79,nyuma ya Andreas Halvorsen wa Denmark aliyeshinda dhahabu kwa dakika 8 sekunde  20.56.

Mwingereza Edward Bird alishinda medali ya shaba, huku Mkenya mwingine Clinton Kimutai akiambulia nafasi ya 11 .

Awali Diana Chepkwemoi alizoa nishani ya shaba kwenye fainali ya mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa wanawake, akiweka muda bora wa kibinafsi wa dakika 9 sekunde 29.84.

Sembo Almayew  wa Ethiopia alinyakua dhahabu akisajili rekodi mpya ya mashindano hayo ya dakika 9 sekunde 12.71, huku Loice Chekwemoi wa Uganda akishinda fedha kwa dakika 9 sekunde 18.84.

Sharon Chepkemoi pia wa Kenya aliridhika na nafasi ya saba .

Ilikuwa  maya ya pili kwa Kenya kupoteza taji hiyo  ya wanawake  katika makala 10 tangu shindano hilo lijumuishwe kwa chipukizi.

Awali jana Mercy Chepkemoi na Marion Jepng’etich, walijikatia tiketi kwa fainali ya mita 3,000  itakayoandaliwa leo.

Mercy ambaye ni bingwa wa kitaifa aliongoza mchujo wa kwanza kwa  muda wa dakika 9 sekunde 22.72, huku Marion pia akiongoza mchujo wa pili kwa dakika 8 sekunde 52.25.

Bingwa wa Afrika Sarah Moraa alifuzu kwa fainali ya mita 800, akishinda mchujo wa tatu wa nusu fainali kwa kutumia dakika 2 sekunde 3.44.

Sarah Moraa akishiriki nusu fainali ya mita 800

Kelvin Kimutai na Phanuel Kosgei pia walifuzu kwa fainali ,Kimutai akimaliza wa pili katika mchujo wa kwanza wa nusu fainali naye Kosgei akaongoza mchujo wa tatu.

Moraa ,Kosgei na Kimutai watarejea kushiriki fainali leo usiku huku Kenya ikilenga kutwaa nishani zaidi.

Kenya ni ya sita kwenye msimamo wa nishani kwa dhahabu 1 fedha 1 na shaba 1.

Ethiopia inaongoza kwa dhahabu 2 na fedha 2,ikifuatwa na Afrika Kusini kwa dhahabu 2 ,fedha 1 na shaba 1 ,wakati Australia ikishikilia nafasi ya tatu kwa dhahabu 2 na shaba 2.

Mashindano hayo yanayowashirikisha wanariadha 1700 kutoka zaidi ya nchini 130 yatakamilika siku ya Jumamosi .

 

Share This Article