Kipindi cha Kenya kiitwacho Kash Money kinapangiwa kuzinduliwa kwenye jukwaa la Netflix mwezi huu wa Januari mwaka 2025.
Kimeandaliwa na kuelekezwa na Phil Bresson na Grace Kahaki na ni simulizi kuhusu siri, usaliti na mienendo mibaya ya familia moja tajiri.
Wawili hao ndio waliandaa kipindi kilichopendwa na wengi kiitwacho ‘Single Kiasi’.
Waigizaji waliohusishwa wanajumuisha mwanamuziki Sanaipei Tande, Lenana Kariba, mtangazaji Makbul Mohamed, John Sibi Okumu, waliokuwa watangazaji Janet Mbugua na Joey Muthengi kati ya wengine wengi.
Kinafichua pia masuala kama ulafi na tamaa na mambo ambayo watu hufanya kwa sababu tu ya pesa.
Jukwaa hilo la Netflix hata hivyo halijatangaza tarehe kamili ya uzinduzi wa kipindi hicho, lakini limethibitisha ni mwezi huu.
Habari za ujio wa kipindi hicho zilitolewa na kampuni ya Insignia Productions kwenye akaunti yao ya Instagram.
Hii sio kazi ya kwanza ya sanaa ya uigizaji ambayo inawekwa kwenye jukwaa hilo la video mitandaoni bali kuna kazi zingine humo kama ‘Mpakani’ na ‘Queen of the North’.