Bingwa mara mbili wa Olimpiki Eliud Kipchoge, ameshinda taji ya tano ya mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani akihifadhi ubingwa wa mwaka jana kwa muda wa saa 2 dakika 2 na sekunde 42.
Kipchoge anayeshikilia rekodi ya dunia ya saa 2 dakika 1 na sekunde 9 aliongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kuhifadhi taji yake.
Chipukizi wa Kenya Vincent Kipkemoi amemaliza pili kwa saa 2 dakika 3 na sekunde 13 huku Tadese Takele wa Ethiopia akiambulia nafasi ya tatu.
Kipchoge aliye na umri wa miaka 38 ameshinda mataji matano ya Berlin katika makala sita aliyoshiriki huku ushindi wa Jumapili ukiwa wa 19 kwa jumla.

Tigist Assefa wa Ethioipia alihifadhi taji ya mwaka jana akiweka rekodi mpya ya dunia ya marathon ya saa 2 dakika 11 na sekunde 53,akivunja rekodi ya Brigid Kosgei miaka minne iliyopita.
Sheila Chepkirui,wa Kenya amemaliza pili kwa saa 2 dakika17 na sekunde 49 wakati Shauri, Magdalena wa Tanzania akitwaa nafasi ya tatu.