Mwanamuziki wa Uganda King Saha amemtetea mwanamuziki mwenza ambaye pia na mwanasiasa Bobi Wine dhidi ya tuhuma za mwanamuziki Eddy Kenzo.
Kenzo alikuwa amedai kwamba Bobi Wine ni tatizo na kikwazo kikubwa katika tasnia ya muziki nchini Uganda.
Kupitia kitandazi cha X, Saha alimwonya Kenzo ambaye ni rais wa chama cha wanamuziki wa Uganda na mshauri wa Rais kuhusu wabunifu, akome kumhusisha Wine kwenye mazungumzo yake.
Saha na Kenzo walitumbuiza kwenye tamasha moja hivi maajuzi katika kile kilichochukuliwa na wengi kuwa kuzika uhasama kati yao.
Kulingana na Kenzo hatua ya Bobi Wine ya kuingilia siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge ndiyo ilisababisha serikali iangazie zaidi wanamuziki na kuwawekea sheria kali.
Kenzo alimlaumu pia Wine kwa kurejelea wanamuziki kama omba omba pale wanapokwenda kuomba misaada ya kifedha kwa wanasiasa.
Awali Bobi Wine ambaye alikuwa akizungumza na wanahabari nyumbani kwake katika wilaya ya Wakiso, alitetea matamshi yake akisema kwa kupokea fedha kutoka kwa viongozi wa kisiasa, wanamuziki wanasaliti mashabiki zao.
“Nilionya kwamba hawa watu watawafanya muwe omba omba na mmalizie kudharauliwa na wale ambao walikuwa wakiwaenzi kikweli.” alisema Bobi Wine.
Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi aliendelea kusema kwamba viongozi hao wa kisiasa wananyanyasa wananchi wa Uganda ambao wanapenda muziki wa wanamuziki wa Uganda kwa sababu unaangazia shida zao.