Wanandoa maarufu nchini Kenya King Kaka na Nana Owiti wametangaza utengano wao, baada ya miaka 13.
Wawili hao walichapisha taarifa ya pamoja kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii ambapo walifungua kwa kusema kwamba hawakudhania wangewahi kutoa taarifa kama hii.
“Baada ya kutafakari sana, tumeafikia uamuzi mgumu wa kuhitimisha uhusiano wetu.” ilisema taarifa hiyo huku ikitaja mazuri waliyoshiriki hasa malezi ya watoto wao watatu.
Wanasema malezi ya watot hao yatasalia kuwa muhimu kwao, ndiposa watasalia na uhusiano wa kirafiki wa heshima.
“Kama watu maarufu, tunatambua kwamba maisha yetu yanaweza kuvutia umma lakini tunaomba mtuelewe na mtuachie usiri wetu, tunapopitia mabadiliko haya.” ilisema taarifa hiyo.
Nana na Kaka wanasema watasaidiana kulea watoto wao kwa mapenzi, uthabiti na heshima kwani watoto wao ni wa muhimu sana.
Wamefafanua kwamba wamekubaliana fika kuchukua hatua hii na wanashukuru wote wanaoheshimu ufaragha wao.